Saturday, May 27, 2006

Blogu ya Mazingira Imefumika

Alan wa saalan wanablogu na wasomaji blogu. Ukimya uliojitokeza ulishadidiwa na safari ndefu kutoka Paterson, New Jersey hata Dar es Salaam, Bongo. Bado inaendelea kuelekea Mbeya.
Bongo shwari hakuna shari. Pengine majambazi yamehisi kuwa wenye pesa zao sasa ni waangalifu zaidi. Pia yawezekana majambazi hayo bado yanakula faida kwanza.
Kufika Bongo nikakutana na rafiki yangu Alexander Mwalyoyo kashawishika na kukata shauri kuanzisha blogu ya Mazingira. Yeye hataki kuitukanisha taaluma yake ya mazingira. Sasa mazingira ndio nini na yanafaa nini katika kublogu. Mie maamuma lakini nikamtembelea Mtanganyika huyo hapa ili kujua vema.
Wakatabahu.

Wednesday, May 17, 2006

Kwaheri Marikani

Hivi leo namalizia rasmi maisha yangu hapa kwa Dubya. Heri safari ndefu ya maisha haya imegota salama na kwa amani. Maulana ashukuriwe. Panapo majaaliwa nitakuwa nikiblogu kutokea hapa katika jiji hili. Ni upande mwingine wa shilingi tu.

Alamsik Binuur

Sunday, May 14, 2006

Nalo Liko Kivya-kevyake

Hili nalo halingoji. Liko mtandaoni kivyake-vyake. Limekaaje? Mwenye macho haambiwi tazama hapa.

Saturday, May 06, 2006

Hii Imekaa Vipi
Majuzi ilikuwa siku ya uhuru (ama ufungwa) wa vyombo vya habari duniani. Martha Mtangoo na Reginald Miruko walikuja na machapisho bloguni kuhusi siku hii. Suala kuu litandalo mawazo ya wanahabari ni kuwa je kuna uhuru kweli ama vinginevyo. Kama uhuru huo umenyakwa nani basi anaunyaka serikali ama waandishi wenyewe. Je, tuzilaumu serikali kupora uhuru huo ikiwa fika tunafahamu kuwa, kwa mfano Tazania, vyombo hivyo kwa urali fulani vimegeuka visemeo vya serikali badala ya chachu ya kuuliza kwa niaba ya wananchi. Kupigia baragumu serikali hasa kwa yale hata yasiyostahiki sio hatua ya awali kujipora wenyewe uhuru huo. Lakini pia mnamkumbuka Hayati Katabalo?
Huo ulikuwa mwanzo tu wa kuingia katika katuni hizi hapa chini kuhusu suala zima la uhuru ama ufungwa wa vyombo vya habari. Nimezifuma katika kusakasaka masuala mbalimbali mtandaoni. Unajua tena unapokuwa huna la maana sana la kufanya.
Unamkumbuka Chakubanga? Zake na nyingine nyingi tu za watanzania wenzetu zinapatikana hapa.

Alamsik Binuur.

Wednesday, May 03, 2006

Miujiza ya Ki-Yesu Yesu Bongo

Nani kakwambia ni Yesu pekee aliweza kufanya miujiza ya kugeuza mikate na samaki wachache na kuwa chakula cha maelfu. Nani kakudanganya ni Yesu pekee alifufua wafu, kuponya wagonjwa na miujiza mingine lukuki. Bongo kuna muujiza umetokea wa kujenga shule zipatazo 381 kwa miezi minne tu! Sio kuendeleza zilizokuwapo. Hapana. Mpya 381 ndani ya miezi minne!. Kama unabisha fungua hapa.