Sunday, March 26, 2006

Blogu ya Kiswahili ya Mkenya David Kiyeu Imekamilika
Pengine tunasahau hata kule Kenya Kiswahili chatumika. Basi kudhihirisha hili mwalimu wa Kiswahili kutoka Kenya anayefanya shughuli zake kule Rhode Island, David Kiyeu, 'amekata shauri' na kuona kuwa chelewa chelewa unaweza kukuta mwana si wako. Kama ilivyo ada ya waswahili mgeni siku ya kwanza tunamkaribisha kwa bashasha. Hebu tukamsalimie hapa.

Friday, March 24, 2006

Mija Kategua

Pengine haikua na maana sana kupost picha ya wanamuziki mashuhuri hapo chini. Lakini kilichonipemba ni kupima ufahamu na kumbuumbu miongoni mwa watembeleaji wa kibaraza changu hiki. Kamtihani haka kalinikumba binafsi nilipoiona kwa mara ya kwanza.

Hatimaye nimeng'amua kuwa uwezo wa kumbukumbu wangu katu hauufikii ule wa mwanadada Mija Sayi. Msanii huyu bwana sio mchezo. Yeye kanitegulia kikamilifu.

Hao jamaa ndio hasa waliokuja kuwa maarufu duniani kote. Nakumbuka hata pale Mbeya Secondary School tukishindana kupata mashairi ya Bob Marley(pichani juu) ili mosi tuweze kuzielewa nyimbo zake lakini pili tufuatilie midundo ile. Yastaajabisha miaka inavyokwenda kasi namna hii hata sasa natamani kurejea maisha yale ya kishule-shule. Kwenye chapisho lililopita Bob anaonekana kushoto na tabasamu lake aliloendelea nalo hata baadaye. Kansa ilimtanguliza Bob kunako jicho la haki mwaka 1981.

Bunny Wailer (pichani kushoto) ndiye anayeonekana kwenye picha ya chapisho lililopita akiwa katikati. Ndiye mwenye jina lililotumika kuanzisha The Wailers. Bunny Wailer bado anadunda kule Jamaica.

Peter Tosh (pichani kulia) ndiye anayeonekana mrefu kuliko wenzie kulia katika picha ya chapisho la chini. Yeye ndiye aliyekng'utwa risasi na majambazi mwaka 1987 nyumbani kwake Jamaica. Huyu baadaye alijiengua kutoka The Wailers na kuanza kivyake. Mbali na kuwa watu 'walifahamu' kuwa alikuwa-ga anatumia-ga 'lile jani', yeye alikuja hadharani na kulitetea kuwa lihalalishwe.

Pichani chini ndipo wote watatu walipoanzisha The Wailers mwaka 1964. Zingine zipo hapa.

Saturday, March 18, 2006

Leo Ninawatega!
Hii picha ni ya vijana wadogo miaka hiyo, ambao baadaye walikuja kuwa wanamuziki mashuhuri duniani kote. Nyimbo zao ni maarufu kama majina yao. Waliunda bendi iliyoitwa kwa jina la mmoja wao. Mmoja wao alipigwa risasi mwaka 1987. Ni akina nani hawa?

Sunday, March 12, 2006

Twaweza Kujivuna Kifua Mbele Kuwa Sisi ni Nani? Mavazi Yatosha.

Alan wasaalan wapendwa wanablogu za Kiswahili. Leo nimekuwa bussy kidogo na vijishughuli vyangu hapa mtoni. Laini sio sana maana ufundishaji wangu hapa ni kama niko likizo fulani vile. Nina wanafunzi wachahe ukifananiaha na wale wastani wa 500 ninaokuwa nao kila mwaka pale kijiweni kwangu Mbeya (zamani DSA).

Nimekuwa na wakati mgumu hapa Marekani kwa masuala kadhaa. Mengi ya hayo ni kawaida inapokuwa unabadilisha tamaduni na mazingira. Bahati njema mengi nemeshayazoea na sasa na dunda kama 'kawa' tu. Kwa mfano masuala ya kutafuna misosi yao hii lilikuwa taabu tupu. Lakini sasa natafuna tu pasi na matatizo.

Langu leo sio geni sana. Lahusiana sana na hii hali ya hewa hapa Marekani ya kaskazini. Kwa kawaida sehemu hii ya nchi ni baridi sana kuliko kule kusinikusini aliko Boniphace Makene, lakini sio kama baridi ya kule aliko mpare huyu. Makene aliniambia-ga huwa-ga anavaa-ga kaptura tu na kuingia mtaani. Thubutu kuvaa kamptura hapa New Jersey halafu uingie mtaani. Unaweza kushangaa ghafla umezingirwa na gari la zimamoto, gari la wagonjwa na na lile la polisi kwani 'msamalia' mmoja anaweza kuwa amewapigia simu na kuwaambia kuna 'punguani' sehemu fulani. Kitakachofuatia sio maswali bali ni msobemsobe mpaka Intensive Care Unit kukupima ubongo na akili yako. Mpaka kugundua kuwa wewe si hamnazo ni tuu leti.

Pengine hili ni kati ya yale mauza-uza ambayo abadani sitaweza kuyazoea hapa Marekani ukizingatia kuwa hata hivyo wasaa wangu wa kusalia hapa umebaki mfupi tu. Si punde nitakuwa Dar ama Mzizima kucheza Twanga Pepeta (Original au Chipolopolo) nikiwa njiani kupitia Mikumi, milima mizuri ya Udzungwa na Kitonga kuelekea jijini Mbeya.

Baridi haizoeleki ati. Hata wazawa wa hapa si tu hawaipendi bali pia wanaichukia kama nini. Je itakuwaje kwa mpitanjia kama mimi.

Nilipokuwa nakaribia kuja huku Marekani sikuelewa vema mabalaa nitakayoyakuta hasa kuhusu hii baridi Nikabeba vijinguo vyangu ninavyovaa-ga Dar na Mbeya. Nikakusanya vishati vyangu vya batiki, tena vya mikono mifupi. Hata hivyo niliwahi kupata fursa yakuvivaa kabla dholuba haijatamalaki pale Novemba. Nilichelewa kuyavaa yale mashuka ya kimasai ingawaje mimi ni (bashiri mwenyewe).

Ninachotaka kujadili hapa ni utambulisho tunaokuwa nao miongoni mwa watu wa mataifa mbalimbali kutokana na mavazi yetu. Nakumbuka wazungu wakizimia vivazi hivi na kusema, "Your shirt is so beautiful John." Hawakuishia hapo: "When you go back to your country I need two like those." Nikawa nimefanikiwa kupeleka ujumbe.

Juma la pili akaja jamaa mweusi kama mimi nilipokuwa nimekaa. Alijawa na bashasha dhahiri kuniona. Kabla hata ya kunisalimia swali lake lilikuwa: "Where in Africa do you come from brother?" Baadaye ndipo akaniambia kuwa anatoka Nigeria. Mavazi yangu ndio pekee yaliyomfanya anitambue natoka wapi. Hakika kichwa kilivimba wakati ule kabla ya msimu wa baridi haujaanza. Nguo zote unazozipenda zinakuwa ndani ya koti zito, pengine usizivae kabisa kwani hazitangamani na makoti yao hapa. Mnigeria mwingine aliyevaa kama Rais Olusegun Obasanjo (pichani juu)aliniambia kule Washington kuwa mavazi ya kikwetu yanatutofautisha na kutuonyeasha sisi ni kina nani na wapi twatoka.

Siku moja tukibung'aa bung'aa jijini New York jamaa mmoja wa kutoka Israel akanishawishi nininue fulana imeandikwa "I love New York." Kuepusha shari nikamwambia "Siipendi New York ila kama utaniuzia iliyoandikwa 'I love Jerusalem' au 'I love Tel aviv' nitanunua."

Napenda sana mavazi ya kikwetu kama hilo alilivaa Da'Mija Shija (pichani kushoto, kwa hisani ya albamu yake). Pia hebu angalia ninavyotofautiana na huyu mlezi wangu hapa mtoni (pichani chini ya hiyo ya Olusegun). Vyetu vizuri jamani na tuvipende basi walau mara moja moja. Yafaa nini sisi tuwe kama hatuna kwetu wakati watu wa kutoka mfano China, Nigeria, Uarabuni na kwingineko wanawakilisha.

Friday, March 10, 2006

Utumwa Mkomavu
Alan wasalan wapendwa wanablogu za Kiswahili katika kibanda changu hiki. Leo sina jipya sana isipokuwa nimevumbua uvundo ambao umekuwa katika ubongo wangu ng’oya huu. Leo nataka nitoe duduku langu juu ya sisi kuendelea kutumia majina ambayo pengine tulipewa kwa kubezwa na watawala wetu mbalimbali pasi na sisi kutambua hivyo. Tanabahi naongelea kuhusu majina sio maneno.

Mwezi uliopita Serikali ya Afrika ya Kusini iliamua kurejesha jina la kitongoji kimoja cha Soweto cha Sopiatown kutoka jina la Triomf (Shangwe). Jina hili lilibadilishwa na madhalimu wa ubaguzi wa rangi mnamo miaka ya 1960 baada ya bomoabomoa Sophiatown na kujenga makazi ya wazungu. Walikuwa na ‘shangwe’ ya kubomoa na kuwafukuzia mbali weusi, watu wasio na maana mbele ya macho ya wazungu. Waweza soma vema vuguvugu hili hapa na hapa. Ukitaka uelewe vema maisha yalivyokuwa katika kitongoji hiki msome hayati Can Themba (pichani kushoto) katika mkusanyiko wa riwaya zake fupi-fupi The Will to Die (hicho kulia)

Kule India kuna mvuvumko huu wa kubadili majina waliopewa wakati wa ukandamizajia wa kutoka nje ya nchi yao. Walianza kubadilisha Madras, na Calcutta na hivi karibuni Mumbay kutoka Bombay. Tazama sababu hapa. Hawajaishia kwenye jina la jiji tu bali hata mitaa yake. Piga chabo hapa.

Mifano ipo mingi kuanzia huko Afrika ya Kusini mpaka India na hata Congo Kinshasa ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama Zaire. Msukumo wangu hapa ni katika jina la jiji letu maarrufu ingawaje halina umeme na maji vya kutosha, Dar es Salaam (pichani kushoto). Chetu ni chetu hata kama ni kichafu. Nikiwa hapa Marekani huwa napata shida kuitangaza Tanzania na Dar es Salaam. Hata hivyo kuna baadhi ya watu wamewahi kusikia-sikia ‘Tanzania’ na ‘Dar es Salaam.’

“It’s a beautiful city,” huwa najitutumua kuwaabia ili wanielewe natokea wapi ingawaje moyoni najua fika kuwa natokea Mbeya na kuwa Dar sio ‘biutifuli’. Hebu pita Kariakoo peke yake na uone jinsi utakavyolazimika kuruka maji taka yanayotoka kwenye nyumba wanazokaa wahindi.

“Actually the name means ‘Heaven of Peace’ as was dubbed by a Zanzibar Sultan more than a century ago,” naendelea bila kufafanua u-heaven ulimaanisha nini kwa Sultani na ‘peace’ ilimaanisha nini.

Hapa ndipo huwa nakuwa na kigugumizi. Sitaki kuendelea kufafanua kuwa kwa Sultani Majid bin Said ilimaanisha sehemu nzuri kwa kutoroshea watumwa. Huwa nachelea kurefusha mjadala na pengine kuepuka kuonekana naleta hoja za ubaguzi wa rangi. Mwafrika hapa Marekani huna maana ati ingawaje watakufanya ujione una nafasi miongoni mwao.

Kwa Sultani kutorosha watumwa, babu na bibi zetu, kupeleka kuwauza katika mashamba ya sukari visiwani Reunion na wengine kuwapeleka uarabuni kwa kazi za uyaya ilikua “Mbingu (bandari) ya Amani”. Ilikuwa vema sana kwa waarabu kuvua utu wetu na kutufanya kama ngombe maksai wa kulima sukari na kuchota maji. Hapa nakumbuka kipengele kichungu sana baina ya utumwa wa kizungu wa Afrika ya magharibi na wa kiarabu uliokuw Afrika ya mashariki. Ukitembelea hapa Marekani utakutana na wamerekani weusi waliotokana za kizazi ha watumwa kutoka Ghana, Ivory Coast, Togo, Nigeria na kwingineko. Umeshawahi kuwaona watu kama hawa Muscati, Dubai, Abudhabi, Jeda na kwingineko? Walikuwa wakiwahasi ili kuhofia 'kuwapitia' wake zao watakapokua safarini Afrika ya mashariki.

Hoja sasa: yafaa nini tuendelee kuita jiji letu hili kwa jina linalokumbusha na kuhuisha machungu ya utumwa. Au kwa kuwa hatukufanyiwa sisi basi twaona ni vema tu. Yapo majina lukuki kama vile Ziwa Victoria, Safu za milima ya Livingstone na kadhalika. Lakini yafaa sasa tufikirie kama India na Afrika ya kusini kuanza kubadilisha majina haya. Tena Dar es Salaam ilikuwa na jina zuri tu kabla ya Sultani: Mzizima, likiwa na maana “mji wa afya.” Angalia vema hapa na hapa. Kuendelea kujidai kuwa unatoka 'Dar es Salaam' sio kuendeleza na kuutukuza utumwa?

Ni swali tu.