Friday, March 10, 2006

Utumwa Mkomavu
Alan wasalan wapendwa wanablogu za Kiswahili katika kibanda changu hiki. Leo sina jipya sana isipokuwa nimevumbua uvundo ambao umekuwa katika ubongo wangu ng’oya huu. Leo nataka nitoe duduku langu juu ya sisi kuendelea kutumia majina ambayo pengine tulipewa kwa kubezwa na watawala wetu mbalimbali pasi na sisi kutambua hivyo. Tanabahi naongelea kuhusu majina sio maneno.

Mwezi uliopita Serikali ya Afrika ya Kusini iliamua kurejesha jina la kitongoji kimoja cha Soweto cha Sopiatown kutoka jina la Triomf (Shangwe). Jina hili lilibadilishwa na madhalimu wa ubaguzi wa rangi mnamo miaka ya 1960 baada ya bomoabomoa Sophiatown na kujenga makazi ya wazungu. Walikuwa na ‘shangwe’ ya kubomoa na kuwafukuzia mbali weusi, watu wasio na maana mbele ya macho ya wazungu. Waweza soma vema vuguvugu hili hapa na hapa. Ukitaka uelewe vema maisha yalivyokuwa katika kitongoji hiki msome hayati Can Themba (pichani kushoto) katika mkusanyiko wa riwaya zake fupi-fupi The Will to Die (hicho kulia)

Kule India kuna mvuvumko huu wa kubadili majina waliopewa wakati wa ukandamizajia wa kutoka nje ya nchi yao. Walianza kubadilisha Madras, na Calcutta na hivi karibuni Mumbay kutoka Bombay. Tazama sababu hapa. Hawajaishia kwenye jina la jiji tu bali hata mitaa yake. Piga chabo hapa.

Mifano ipo mingi kuanzia huko Afrika ya Kusini mpaka India na hata Congo Kinshasa ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama Zaire. Msukumo wangu hapa ni katika jina la jiji letu maarrufu ingawaje halina umeme na maji vya kutosha, Dar es Salaam (pichani kushoto). Chetu ni chetu hata kama ni kichafu. Nikiwa hapa Marekani huwa napata shida kuitangaza Tanzania na Dar es Salaam. Hata hivyo kuna baadhi ya watu wamewahi kusikia-sikia ‘Tanzania’ na ‘Dar es Salaam.’

“It’s a beautiful city,” huwa najitutumua kuwaabia ili wanielewe natokea wapi ingawaje moyoni najua fika kuwa natokea Mbeya na kuwa Dar sio ‘biutifuli’. Hebu pita Kariakoo peke yake na uone jinsi utakavyolazimika kuruka maji taka yanayotoka kwenye nyumba wanazokaa wahindi.

“Actually the name means ‘Heaven of Peace’ as was dubbed by a Zanzibar Sultan more than a century ago,” naendelea bila kufafanua u-heaven ulimaanisha nini kwa Sultani na ‘peace’ ilimaanisha nini.

Hapa ndipo huwa nakuwa na kigugumizi. Sitaki kuendelea kufafanua kuwa kwa Sultani Majid bin Said ilimaanisha sehemu nzuri kwa kutoroshea watumwa. Huwa nachelea kurefusha mjadala na pengine kuepuka kuonekana naleta hoja za ubaguzi wa rangi. Mwafrika hapa Marekani huna maana ati ingawaje watakufanya ujione una nafasi miongoni mwao.

Kwa Sultani kutorosha watumwa, babu na bibi zetu, kupeleka kuwauza katika mashamba ya sukari visiwani Reunion na wengine kuwapeleka uarabuni kwa kazi za uyaya ilikua “Mbingu (bandari) ya Amani”. Ilikuwa vema sana kwa waarabu kuvua utu wetu na kutufanya kama ngombe maksai wa kulima sukari na kuchota maji. Hapa nakumbuka kipengele kichungu sana baina ya utumwa wa kizungu wa Afrika ya magharibi na wa kiarabu uliokuw Afrika ya mashariki. Ukitembelea hapa Marekani utakutana na wamerekani weusi waliotokana za kizazi ha watumwa kutoka Ghana, Ivory Coast, Togo, Nigeria na kwingineko. Umeshawahi kuwaona watu kama hawa Muscati, Dubai, Abudhabi, Jeda na kwingineko? Walikuwa wakiwahasi ili kuhofia 'kuwapitia' wake zao watakapokua safarini Afrika ya mashariki.

Hoja sasa: yafaa nini tuendelee kuita jiji letu hili kwa jina linalokumbusha na kuhuisha machungu ya utumwa. Au kwa kuwa hatukufanyiwa sisi basi twaona ni vema tu. Yapo majina lukuki kama vile Ziwa Victoria, Safu za milima ya Livingstone na kadhalika. Lakini yafaa sasa tufikirie kama India na Afrika ya kusini kuanza kubadilisha majina haya. Tena Dar es Salaam ilikuwa na jina zuri tu kabla ya Sultani: Mzizima, likiwa na maana “mji wa afya.” Angalia vema hapa na hapa. Kuendelea kujidai kuwa unatoka 'Dar es Salaam' sio kuendeleza na kuutukuza utumwa?

Ni swali tu.

7 Comments:

At 4:40 PM, Blogger Jeff Msangi said...

Maswali yako kabambe na yanachoma moyoni kwa makali ya aina yake.Nina maswali na majibu kama hamsini kwa hoja hizi.Leo sina muda wa kutosha na hoja kama hizi huwa sipendi kuziachia hewani.Huwa napenda zijadiliwe na kisha mikakati iundwe.Ndio maana mimi huwa sipendelei sana makongamano ambako matatizo huanishwa na watu wakatawanyika,ukiuliza solution!!!Wapi.Mwaipopo nitakurudia katika hili.

 
At 8:40 AM, Blogger boniphace said...

Kun hoja hapa nitarudi baadaye nikiweka kitako. Kazi njema

 
At 5:07 AM, Blogger MICHUZI BLOG said...

alipokuwa akitokea oman kuelekea zenj, sultan said barghash alijikuta analazimika kwenda kusini magharibi kutokana na dhoruba baharini. merikabu yake ilipokaribia pwani ya bagamoyo ikashindwa kutia nanga kwani kina kilikuwa kidogo. safari ikaendelea kusini na kupitia mbweni, kunduchi na hatimaye msasani. kote huko, ukiondoa msasani (ambako pia maji yalikuwa ya ugokoni) dhoruba ilikuwa kubwa. akageuza na kuzunguka peninsula ya msasani na kuelekea kunako mdomo mwembamba ambapo awali yeye na manahodha wake walidhani waelekea ziwani, kwani si mara nyingi kukuta mdomo mdogo wa maji chumvi kiasi kile. walipouvuka mdomo huo (ambao sasa ni kati ya gati la magogoni, wakakuta bahari imetuama kama ziwa. wakaendelea hadi kurasini na kukuta shwari. akaipenda sehemu hiyo na kuipa jina na bandar u salaam, kwa usalama wa maji na sio kwa amani nchi kavu. nadhani nimejieleza vya kueleweka-ga...

kuhusu majina, mnaonaje ziwa viktoria tubadilishe liitwe ziwa i.e. kawawa ama kidude ama kikwete...

 
At 3:47 PM, Blogger John Mwaipopo said...

mimi nimekuelewa. Nashukru kwa elimu hii.

 
At 12:30 PM, Blogger Mija Shija Sayi said...

Unajua sikuwahi kufikiria juu ya hili suala la waafrika waliopelekwa uarabuni kutokuzaana huko kama Marekani ilivyo sasa hivi, kumbe tulikuwa tukihasiwa!!!!
Jamani kuna watu wakatili duniani.

Michuzi,
Kuhusu jina la ziwa victoria, kuna kipindi Ndesanjo alishaandika juu ya hili. Nimeona niwaletee hapa hapa ili kuwalahisishia. Kiungo ni hiki.http://www.jikomboe.com/?p=544
na habari ni hii:-

Mon 14 Feb 2005
HISTORIA YETU: UNALIJUA ZIWA NAMLOLWE?
Na , Maudhui: Uncategorized

Ziwa Namlolwe ni ziwa ambalo hivi sasa, kutokana na ukoloni na utumwa wetu wa mawazo waliotuachia wakoloni, linaitwa Ziwa Vikitoria (Lake Victoria.) Waluo walikuwa wakiliita ziwa hili Namlolwe.
Huyu malkia mwenye ziwa Afrika Mashariki sijui alitufanyia nini watu wa Afrika Mashariki kiasi cha kuamua kulipa ziwa hili jina lake. Hivi kuna ziwa au mto gani kule Uingereza uliopewa jina la Mwafrika?
Kule Zimbabwe kuna maporomoko yanaitwa Maporomoko ya Vikitoria (Victoria Falls). Jina la asilia la maporomoko haya ni Mosi O Tunya (yaani moshi utoao mlio kama radi).

 
At 4:08 PM, Blogger Ndesanjo Macha said...

Tatizo letu moja tuna tabia ya kutazama mambo fulani kama vile hayana uzito wowote. Mtu atasema, jina si jina tu?

Kama jina ni jina tu mbona huko Uropa hukuti mito, maziwa, n.k. vikiwa na majina ya malikia, manabii, "watakatifu," au mashujaa wa Afrika? Kwanini sisi tu ndio tunachukua majina ya wengine kama akina Ziwa Vikitoria? Au mlima Livingstone?

Tazama hata majina ya hoteli zetu, kampuni zetu, maduka yetu...jini ni jina tu?

Njia mojawapo ya kutunza historia, ukiachia mbali zile za kuandika au kuwa na fasihi simulizi, ni kuita vitu majina. Ukiwa na ziwa linaitwa Ngwanamalundi, unakuwa unatunza historia yake maana vizazi vijavyo vinakuja kujiuliza kwanini ziwa hili likaitwa hivi? Wanatafiti, mara wanakutana na historia yake.

Mwaipopo unachokonoa mambo fulani ya msingi sana katika safari ya kujijua na kujikomboa kifikra. Sijui kama kuna aliyesikiliza albamu ya Damian Marley ya Jamrock. Wimbo wa mwisho una hotuba ya Marcus Garvey. Kama umeipata, yule anayesema kuwa tusipoweza kufanya mambo ambayo mataifa mengine yamefanya basi tutaangamia ni Garvey mwenyewe. Msikilize vyema (anaongea kwa haraka ).

 
At 9:29 PM, Blogger Pusat Perkasa said...

vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada
vimax canada

 

Post a Comment

<< Home