Twaweza Kujivuna Kifua Mbele Kuwa Sisi ni Nani? Mavazi Yatosha.Alan wasaalan wapendwa wanablogu za Kiswahili. Leo nimekuwa bussy kidogo na vijishughuli vyangu hapa mtoni. Laini sio sana maana ufundishaji wangu hapa ni kama niko likizo fulani vile. Nina wanafunzi wachahe ukifananiaha na wale wastani wa 500 ninaokuwa nao kila mwaka pale kijiweni kwangu Mbeya (zamani DSA).
Nimekuwa na wakati mgumu hapa Marekani kwa masuala kadhaa. Mengi ya hayo ni kawaida inapokuwa unabadilisha tamaduni na mazingira. Bahati njema mengi nemeshayazoea na sasa na dunda kama 'kawa' tu. Kwa mfano masuala ya kutafuna misosi yao hii lilikuwa taabu tupu. Lakini sasa natafuna tu pasi na matatizo.
Langu leo sio geni sana. Lahusiana sana na hii hali ya hewa hapa Marekani ya kaskazini. Kwa kawaida sehemu hii ya nchi ni baridi sana kuliko kule kusinikusini aliko
Boniphace Makene, lakini sio kama baridi ya kule aliko
mpare huyu. Makene aliniambia-ga huwa-ga anavaa-ga kaptura tu na kuingia mtaani. Thubutu kuvaa kamptura hapa New Jersey halafu uingie mtaani. Unaweza kushangaa ghafla umezingirwa na gari la zimamoto, gari la wagonjwa na na lile la polisi kwani 'msamalia' mmoja anaweza kuwa amewapigia simu na kuwaambia kuna 'punguani' sehemu fulani. Kitakachofuatia sio maswali bali ni msobemsobe mpaka Intensive Care Unit
kukupima ubongo na akili yako. Mpaka kugundua kuwa wewe si hamnazo ni tuu leti.
Pengine hili ni kati ya yale mauza-uza ambayo abadani sitaweza kuyazoea hapa Marekani ukizingatia kuwa hata hivyo wasaa wangu wa kusalia hapa umebaki mfupi tu. Si punde nitakuwa Dar ama Mzizima kucheza
Twanga Pepeta (Original au Chipolopolo) nikiwa njiani kupitia Mikumi, milima mizuri ya Udzungwa na Kitonga kuelekea jijini Mbeya.
Baridi haizoeleki ati. Hata wazawa wa hapa si tu hawaipendi bali pia wanaichukia kama nini. Je itakuwaje kwa mpitanjia kama mimi.
Nilipokuwa nakaribia kuja huku Marekani sikuelewa vema mabalaa nitakayoyakuta hasa kuhusu hii baridi Nikabeba vijinguo vyangu ninavyovaa-ga Dar na Mbeya. Nikakusanya vishati vyangu vya batiki, tena vya mikono mifupi. Hata hivyo niliwahi kupata fursa yakuvivaa kabla dholuba haijatamalaki pale Novemba. Nilichelewa kuyavaa yale mashuka ya kimasai ingawaje mimi ni (bashiri mwenyewe).
Ninachotaka kujadili hapa ni utambulisho tunaokuwa nao miongoni mwa watu wa mataifa mbalimbali kutokana na mavazi yetu. Nakumbuka wazungu wakizimia vivazi hivi na kusema,
"Your shirt is so beautiful John." Hawakuishia hapo: "When you go back to your country I need two like those." Nikawa nimefanikiwa kupeleka ujumbe.
Juma la pili akaja jamaa mweusi kama mimi nilipokuwa nimekaa. Alijawa na bashasha dhahiri kuniona. Kabla hata ya kunisalimia swali lake lilikuwa: "Where in Africa do you come from brother?" Baadaye ndipo akaniambia kuwa anatoka Nigeria. Mavazi yangu ndio pekee yaliyomfanya anitambue natoka wapi. Hakika kichwa kilivimba wakati ule kabla ya msimu wa
baridi haujaanza. Nguo zote unazozipenda zinakuwa ndani ya koti zito, pengine usizivae kabisa kwani hazitangamani na makoti yao hapa. Mnigeria mwingine aliyevaa kama Rais
Olusegun Obasanjo (pichani juu)aliniambia kule Washington kuwa mavazi ya kikwetu yanatutofautisha na kutuonyeasha sisi ni kina nani na wapi twatoka.
Siku moja tukibung'aa bung'aa jijini New York jamaa mmoja wa kutoka Israel akanishawishi nininue fulana imeandikwa "I love New York." Kuepusha shari nikamwambia "Siipendi New York ila kama utaniuzia iliyoandikwa 'I love Jerusalem' au 'I love Tel aviv' nitanunua."
Napenda sana mavazi ya kikwetu kama hilo alilivaa
Da'Mija Shija (pichani kushoto, kwa hisani ya albamu yake). Pia hebu angalia ninavyotofautiana na huyu mlezi wangu hapa mtoni (pichani chini ya hiyo ya Olusegun). Vyetu vizuri jamani na tuvipende basi walau mara moja moja. Yafaa nini sisi tuwe kama hatuna kwetu wakati watu wa kutoka mfano China, Nigeria, Uarabuni na kwingineko wanawakilisha.