Saturday, November 18, 2006

Bado Nadunda Wajameni
Pengine wa-Swahili hunena “Kimya kingi kina mshindo wake” ama “Debe tupu haliachi kuvuma” Kama mie ndilo hilo debe basi sijavuma tena katika utandao huu wa ku-blogu. Vile vile kimya changu katu hakina mshindo. Ni vijimambo tu hapa katikati vimetukia. Na hii haina maana kasi ya kublogu itarejea kama ile ya awali wakati niko kwenye nchi ya asali na maziwa kama Boni Makane apendavyo kuiita.

Bongo inahitaji ubishi kuweza kuiishi. Hili nimebaini baada ya kurejea. Pengine mumekwisha kusikia hali ngumu ya umeme. Mlio ughaibuni hapana shaka mmesoma katika vyombo vya kueneza urongo kama Ndesanjo aviitavyo. Katika hili hakuna urongo hata chembe. Umeme wakatika saa 12 asubuhi na kurejeshwa saa moja jioni. Kwa sasa ni kawaida kuwasikia watanzania ifikapo jioni kuimba kawimbo ambako hata hakana korasi. Kawimbo kenyewe kanaitwa “Umeme umerudi”. Kila familia usaisikia hivyo.

Hayo masaa ya mgao ni jumatatu hata ijumaa. Ukibahatika kupitiwa na laini ya umeme unaokwenda wa vigogo basi waweza kuupata siku mbili tu: Jumamosi na Jumapili.

Stori hii inaanzisha chanzo cha kushindwa kublogu kwangu na wengine wanaoleweshwa na huduma hii. Sikiliza kituko hiki.

Hapa jijini Mbeya tuna vituo vya Inteneti visivyozidi vi-5 hivi. Kama sio sahihi sana Msangi Mdogo nisaidie. Kadri siku zinavyozidi kwenda huko zinakokwenda ndivyo hamasa ya watu hasa vijana kutumia intaneti inashadidika. Kwa hiyo, mosi, watumiaji ni wengi na pili huduma ni chache. Kwa siku za kazi huduma inaanza wakati wa saa moja jioni. Ama upate huduma ya jenereta.

Kichekesho kipo hapo. Pengine umeme upo lakini mawasiliano ya intaneti hayapo (kama Ijumaa iliyopita maeneo nikaayo yalikuwa yamehamaki kupata umeme tokea asubuni. Hamad! Kumbe Makamu wa Raisi alikuwa jijini hapa. Natamani ahamie Mbeya ili tupata-ge umeme kila siku).

Wakati mwingine mawasiliano yapo lakini hakuna umeme. Wakati mwingine vyote havipo. Wakati mwingine vyote vipo ama mtumiaji huna muda ama (niseme?) huna shilingi ya kutosha katika mfuko wako. Shilingi nayo inashuka kwa kasi mpya.

Huduma za mawasiliano ya intaneti imezidi kukamiwa ma mikasa ya aina-aina. Wachuuzi wa huduma hii wanadai malipo yameongezeka huko wanakozitoa-ga. Sijui wapi. Bila buku (1000/=) hujahudumiwa kwa ‘lisaa limoja’ Hii ndio dunia yangu. Lisaa basi liwe lisaa. Mawasiliano huja kwa mwendo wa kinyonga. Balaa tupu.

Kizuri katika yoote haya ni kuwa ‘nshajizoelea-ga’ na hali hii mie. Cha muhimu ni kuridhika na maisha yako. Kwa upande mwingine maisha sio mabaya sana. Sijambo.


Alamsik Binuur.