Tuesday, April 06, 2010

Siku ya Afya Duniani: Malaria tunaifanyaje?

Kesho tarehe 7/4 ni maadhimisho ya siku ya afya duniani. Pamoja na mambo mengine, siku hii kimsingi hutumika kuamsha ufahamu wa magonjwa na maradhi kwa binadamu, ikiwa na lengo kuu la kujikina na kutibu ili kupunguza vifo (ingawaje mwisho wa siku wote tutakufa).

Nataka nijielekeze katika ugonjwa hatari ambao umekuwepo tangu mwanadamu awepo hapa duniani. Malaria ni ugonjwa ambao umekuwa ukiangamiza watu hata kabla ya Ukimwi. Na hata sasa. Kutokana na kuwa tishio kwa maisha ya mwanadamu nadhani kuna watu nje na ndani ya Afrika wamefanya malaria ni biashara.


Mbu akieneza malaria

Juhudi kuu dhidi ya malaria imekuwa ‘Kujikinga na mbu waenezao malaria’. Mie sikatai hoja ya kujikinga na mbu lakini nadhani ni wakati sasa tuamke na tuanzishe kitu kama ‘Tumtokomeze mbu aenezae malaria’. Hivi kwa nini tuhangaike na moshi wakati tunakujua moto uliko?

Ninashawishika kudhani katika suala zima la malaria kuna mkono wa kibiashara zaidi, biashara ambayo viongozi wetu wameingizwa ama kwa kujua ama kwa kutokujua.

Kuna jamii hapa duniani wala hazijui uwepo wa ugonjwa huu, achilia mbali kusikia. Kwa mfano, Marekani ni miongoni mwa nchi zilizoteseka sana na ugonjwa huu hususan kuanzia miaka ya 1900 mpaka mwaka 1949. Soma hapa na hapa. Wamarekani wa leo hawajui kama kuna ugonjwa hapa duniani unaitwa ‘malaria’. Hata madaktari wa huko si wote wanajua uwepo na tiba ya malaria.

Marekani yao ni hadithi ya mafanikio katika vita dhidi ya malaria. Baada ya kuangamiza watu sana, hatimaye walitokomeza malaria kwa kunyunyiza dawa ya DDT kila kona na kutoacha maji yatuame hovyo (kutengeneza miundombinu ya maji mizuri).


Vyandarua vilivyotiwa dawa 'kuzuia' mbu

Hapa ndipo hatuambiani ukweli. Wakati Marekani imefanikiwa kutokomeza mbu kwa DDT sie tunaambiwa DDT haifai na tunakubali na kupiga marufuku matumuzi ya DDT. Suala la kutengeneza miundombinu linaweza kuwa gumu kwetu kutokana na uwezo wa kiuchumi lakini nilidhani ni bora tungeambiwa tunashindwa wapi kuliko kutoambizana ukweli. Kila kukicha ‘Tujikinge na mbu waenezao malaria’.

Nijuavyo mimi vyandarua huwezesha mbu kutong’ata watu kitandani tu. Hatuambiwi kuhushu mbu aliye sebuleni, jikoni, maktaba, chooni na bafuni na kadhalika. Au tunatakiwa tuwe na vyandarua ‘vilivyotiwa dawa’ hata maktaba au sebuleni tukiwa tunacheza karata saa sita usiku? Au ‘mbu aenezae malaria’ ni yule aliyeko chumbani tu?


DDT ikipulizwa marekani kuua mbu wote

Wakati baragumu linapulizwa kwa juhudi zote‘ kujikinga na mbu waenezao malaria’, tunaona mataifa ya magharibi yanavyojenga viwanda vya vyandarua kwao na kwetu, wanavyotengeneza dawa kwao (mfano dawa mseto inatengenezwa Brooklyn, New York). Tunawaona wanapotoa misaada yenye masharti kuwa ni lazima tununue dawa kwao. Ilimradi kila uchao ni kauli mbiu za kuuhangaikia moshi ilihali tunakujua moto uliko.

Ni wakati sasa tuambiane ukweli. Tumeshakufa vya kutosha!

Labels:

2 Comments:

At 12:40 PM, Blogger Yasinta Ngonyani said...

Shukrani kwa kutumbusha kwa siku hii.

 
At 9:06 AM, Blogger Christian Bwaya said...

Maleria dawa yake tunaambiwa eti kulala kwenye neti! Mbu anayesababisha maleria huuma usiku wa manane!

 

Post a Comment

<< Home