Tuesday, March 02, 2010

BARUA KWA WAZIRI WA ELIMU[Nimeitoa taarifa hii Wanabidii Forum. Imenisikitisha. Nimeona niitundike hapa pengine/labda/may be/perhaps/ inawezekana hapa ikaonwa na mtoto mhusika akaonewa huruma.kama ni kweli basi si vema. Picha haiusiani na taarifa hii]

Mheshimiwa Waziri Suala hili imebidi likufikie kutokana na watendaji kushindwa kulishughulikia Suala la Neema Mgongo. Neema Mgongo amemaliza darasa la saba Shule ya Msingi Segerea mwaka 2008. Neema hakufaulu, Neema ana Mzazi mmoja tu yaani mama yake. Mama yake alitamani wanae asome shule ya Sekondari. Siku moja wakiwa Kanisani walitangaziwa kuwa kama kuna mtu mwenye mtoto aliyemaliza Darasa la saba Ampeleke kwenye shule inayofadhili wanafunzi na kwamba mwanafunzi atasoma kwa Tshs 100,000 kwa mwaka. Shule hiyo inaitwa KWETU HIGH SCHOOL liyoko Kunduchi Nje kidogo ya jiji la DSM.

Mama Neema alitakiwa kupeleka Barua ya serikali ya Mtaa, Shule alikosomea. Neema alipokelewa Shuleni hapo na mama yake alilipa Tshs 100,000/ mwaka 2009. Mwaka 2010 Shule hiyo imepandisha ada kutoka Tshs 100,000 hadi Tshs 200,000, Mama Neema akashindwa kulipa kiasi hicho maana hana kipato cha uhakika. Mama Neema aliomba msada serikali za Mitaa lakini hakupata msada hasa kupitia NGOs zinazosaidia Wanafunzi wazazi wao wasio na uwezo.

Katika kutafuta msada akapata habari kuwa Neema Mgongo alifaulu awamu ya pili lakini taarifa hazikumfikia kwakuwa alikuwa akiishi mbali na shule aliyosomea. Mama Neema alifika hadi Segerea Shule ya Msingi kupata Ukweli wa habari hizo. Mwalimu mkuu alimwambia ni kweli alipass kwenda Shule ya Uhuru Mchanganyiko. Mama Neema alikwenda Shule ya Uhuru Mchanganyiko akamwona Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo. Mwalimu huyo alimwambia amechelewa sana nafasi ipo ila nenda kwa Afisa Elimu akupe barua ili tumpokee. Mama Neema akachukua barua kuanzia kwa mjumbe hadi serikali ya Mtaa pamoja na Shule iliyokuwa imemfadhili. Akampelekea Afisa Elimu wa Ilala pale Boma. Afisa Elimu akasema amesoma Shule ya Private hatuwezi kumpokea. Mama Neema akamwomba amejeshee Barua alizompa akakataa kumpatia. Kesho yake akamfuatilia Afisa Elimu huyo karibu mwezi Februari 2010 wote.

Mama Neema aliomba Msaada wa Mjumbe wa Nyumba kumi. Hata hivyo Afisa huyo hakujali aliendelea kuzuia Barua hizo. Siku iliyofuata mama Neema alimwendea tena ndipo alipomtupia baadhi ya Barua hizo, Na kwamba barua ya serikali ya Mtaa na Picha alibaki nazo.

Mama Neema aliamua kwenda Wizarani kumwona Mkurugenzi wa Elimu. Wizarani Gorofa ya tatu alimkuta Mkurugenzi Chumba no 302B. Mkurugenzi huyo kabila Msukuma alimwambia aende kwa DO pale kamata jambo hilo litatatuliwa. Mama Neema alikwenda kwa DO, DO alimwambia aende Shule alikosomea Mtoto kamati ya Shule iandike barua alafu aipitishie kwa Afisa Elimu wa Ilala alafu iende kwake. Mama Neema kwa ajili ya mwanae alifuatilia barua Shule alikosoma. Kamati ikakutana na Barua ikaandikwa akapewa mama Neema akaipeleka kwa Afisa Elimu wa Ilala. Afisa huyo akaiangalia akamwambia mama Neema ipeleke kwa DO. Mama Neema aliipeleka kwa DO na DO akakubali akamwambia Mama Neema Mpelekee Afisa Elimu. Mama Neema alifikisha ile barua kwa Afisa Elimu. Afisa huyo akaipokea na kutoa sauti ya kufoka kuwa haiwezekani nimekuambia. Peeeeleka hio barua kwa DO wako. Akaendelea kufoka iache hapo nitamwandikia DO mimi mwenyewe.

Barua imekwamia kwa Afisa Elimu. Hivi DO na Afisa Elimu Mkubwa ninani? MTOTO HUYO YUKO NYUMBANI ANATAKA KUSOMA ANALIA KILA SIKU.

Labels: , ,

4 Comments:

At 9:17 AM, Blogger Masangu Matondo Nzuzullima said...

"Mkurugenzi huyo kabila Msukuma alimwambia aende kwa DO pale kamata jambo hilo litatatuliwa..."

Usukuma wa Mkurugenzi unahusikaje na sakata hili? Wasukuma ndiyo mabingwa wa kutuma watu kwenda kwa DO au???

Danadana kama hizi mbona ni za kawaida? Kuna wakati nilihitaji cheti cha kuzaliwa, mbona ilikuwa kasheshe? Anzia kwa balozi wa nyumba kumi, nenda kwa mkuu wa kitongoji, kata halafu Mkurugenzi wa Wilaya. Halafu nenda mkoani Shinyanga...mwishowe nilikata tamaa!

Nadhani kila mmoja wetu ana mikasa kama hii. Ndiyo jamii yetu inavyofanya kazi na sijui mambo yatabadilika lini. Hatutaweza kuendelea kwa utenda kazi wa aina hii.

Nadhani huyo Mkurugenzi Msukuma mwenzangu atakuwa ameshakisikia kilio cha huyu mama na natumaini kwamba huyu mtoto atasoma bila wasiwasi wo wote!

 
At 9:36 AM, Blogger John Mwaipopo said...

nadhani (simtetei) mwandishi alikuwa anatamani kumbainisha mkurugenzi huyu na mwingine, pengine asiye msukuma. lakini huu ukiritimba tunao watanzania karibu wa makabila yote.

 
At 12:47 AM, Blogger chib said...

Habari hii nimeipokea kwa hisia mbili tofauti, kwanza hasira kwa hao wanao msumbua mama huyo bila sababu, na pili kwa masikitiko kwa Neema ambaye anaelekea kupoteza tena mwaka wa masomo wakati nafasi yake ipo wazi.
Nakumbuka kuna wakati fulani waziri fulani ambaye hatunaye tena aliwahi kukung'utwa na mwananchi aliyechoka kuzungushwa. Yaelekea na huyo afisa elimu anakaribisha jambo hilo.

 
At 1:21 PM, Blogger Mija Shija Sayi said...

Yaani tunazibiana hata katika mambo muhimu kama Elimu, Kweli Tanzania ni ng'ombe wa masikini. Kila siku mimi nasema utawala huu ulikitakiwa upinduliwe kije kitu kingine kabisaa. Yaani kwa ufupi watanzania tunahitaji mtu kama Idi Amini.

 

Post a Comment

<< Home