Wednesday, March 03, 2010

MAJIBU YA SAFARI YA MWANAHABARI MBEYAKamnara ketu

Nimebahatika kutumiwa e-mail ambayo mwandishi wake ameiita ripoti ya safari yake ya kikazi mkoani Mbeya. Ameituma kwa watu wengi ili kueneza uchafu aliouona mkoani humu. Sina uhakika nani alimpa kazi ya kuandika ripoti yake hii maana nijuavyo riporti ina kitu kinaitwa terms of reference yaani waliokutuma na jinsi walivyokutuma kufanya uchunguzi/utafiti. Lakini haidhuru pia inaweza kuwa ripoti binafsi ya muhusika anayejiita mwanahabari, ingawaje ripoti yenyewe inaonyesha alichokiandika sicho alichotumwa kufanya huko mbeya. Waweza isoma hapa
Awali napenda kumpongeza mwanahabari kwa kuonyesha yale ambayo kwa mtazamo wake hayaonwi ama hayajaonwa na watu wasiowahi kufika Mbeya ila nitachukua fursa kidogo kurekebisha yale ambayo yamewasilishwa ndivyo sivyo. Napenda ijulikane mie ni mkaazi wa mbeya kwa karibu miaka 20 mfululizo isipokuwa nikiwa shule ama vyuoni, ambako nako nilitambulika kuwa natoka Mbeya. Hivyo itambulike nina maslahi na uenyeji/ukaazi wangu hapa Mbeya.

Juhudi hii ni kwa ajili ya kuweka sawa kumbukumbu na taarifa kamili. Pili nadhani itamuongezea ufahamu bwana mwanahabari. Tatu juhudi hii itafanya upotoshajia wa makusudi wa mwanahabari pengine kutokana na wembamba wa uwezo wake wa kufikiri, kupembua na kuchanganua mambo, ujulikane.

Nianze na kunukuu mwanzo wa report yake hii. Nanukuu “Duniani kuna mambo mengi sana.” Nukuu hii inaonyesha jinsi gani huyu mwanahabari (lakini mwanahabari aliyetumwa kwenda kutengeneza mashine mbeya. Habari na umakenika wapi na wapi) alivyo maamuma wa kujua mambo hata yaliyo ndani ya nchi yake. Kwake Mbeya tu ni dunia nyingine kabisa! Kwake ilikuwa safari ya kustaabisha eti. Kwa mtu aliyefanikiwa kusafiri kuliko mwanahabari-makenika Mbeya haitofautiani sana kwa raha na mauzauza utakayoyakuta mikoa mingine, pengine mikoa mingine imeizidi hiyo Mbeya. Nitaonyesha kwa kifupi hapa chini.

Kimojawapo ni uwingi wa makanisa na sehemu za kuabudia hapa Mbeya. Eti kutoka kanisa moja mpaka lingine ni hatua 30! Nimekaa Mbeya karibu miaka 20 sijayaona hayo makanisa na viwanja vya kuabudia vilivyopakana hatua 30 kama mwanahabari-makenika anavyotaka kuwadanganya watu ambao hawajafika Mbeya.

Jambo la msingi lililonisukuma sana kujaribu kujibu ripoti hii ni maambukizi ya ukimwi mkoani Mbeya. Ni kweli Mbeya i miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa maambukizi ya gonjwa hili hatari lakini haiifuatii Johanesburg kwa maambukizi. Hata hapa Tanzania tu haishiki namba moja. Soma hapa uhakikishe. Labdha atuambie takwimu hizi kazipata wapi.

Ingawaje ripoti hii ina nia ya kutukumbusha kujiepudha na kujilinda na ukimwi lakini imejaa kejeli kama vile Mbeya na Ukimwi ni sawa na samaki na maji. Kwa mfano anasema “wenyeji wa hapa wengi hawaamini kama kuna ukimwi. Wanaamini mtu akifariki basi amefariki kutokana na mungu (sic) kumwita amechoka maisha ya dunia , wengine ndio hizo imani zao akifa mwenzao amelogwa na mambo kama hayo .” Hivi tujiulize ni kweli asilimia kubwa ya watu wa Mbeya hawajui lolote kuhusu ukimwi isipokuwa wachache na pengine wageni wanaokuja kutengeneza mashine? Kumbuka hapa alipofikia kabla hajaenda Tukuyu (alikokuita ‘mkoa’ paragrafu ya 32) na Kyela ni mjini ambako ufahamu wa uwepo wa ukimwi ni mkubwa. Au amesahau Mbeya kuna watu wanaotoka mikoa yote ya Tanzania na si kweli kuwa wote wana imani za kizamaani za washamba wa Mbeya? Kuna wachagga, wahaya, wamasai, wasukuma, wakwere n.k. Na kabila lake ‘walistaarabika’ nao wapo wanaishi hapa, na wengine hawana mpango wa kurudi huko kwa ‘wastaarabu’.

Mwanahabari-makenika anaanika kuwa hapa Mbeya “ukikutana na wasichana 5 basi 3 wanamarafiki wa kiume ambao sio wanafunzi wenzao yaani watu wa nje tu , wamachinga na madereva au watu wa shuguli zingine , hii inaadhiri sana hawa vijana utendaji wao madarasani” (para 24). Nadhani anaongelea wanafunzi lakini hajatuambia takwimu hizi amezitoa wapi ama lini yeye binafsi alifanya utafiti huu. Na pia sidhani mmomonyoko huu wa maadaili miongoni mwa wanafunzi uko Mbeya tu. Pengine kwao hamna huu upuuzi, upuuzi ambao katu siupigii upatu kokote kuwako.

Nina mashaka na tabia binafsi za mwanahabari-makenika hususani katika masuala ya ngono. Nadhani ni muumini mkuu wa kuendekeza ngono. Pengine kafikia ushemasi kabisa. Inakuwaje mtu ambaye si muendekeza ngono ukachombezana kwa simu kimahaba na wanawake asiowajua hata wakapanga siku ya kwenda Mbeya ili wakapene hilo joto (para 11) alafu anaingia mitini dakika ya mwisho. Au sitaki nataka? Pia inakuwaje mtu asiye mzinzi akaongea na msichana asiyemjua kwa masaa mawili na wakatongozana (para 38) kisha unajifanya kuingia mitini. Nashawishika kuwa mwanahabari-makenika alikuwa akina sitaki-nataka. Nilidhani mtu asiye mzinzi, kama mwanahabari-makenika anavyotuaminisha, asingejihusisha na mazungumzo yanayoshadidia ngono. Nadhani angekuwa mkali mara moja! Tena katika hili anadiliki kuwadhalilisha wasichana wa Mbeya (pasi na kuwa na uhakina ni wenyeji wa kuzaliwa hapa) kuwa ni heri atongoze ng’ombe au mbuzi kuliko wao! (para 40 & 41).

Katika mambo yote aliyoyaona Mbeya, mazuri na mabaya, aliona la ngono ndio kuu. Afrika Kusini pamoja na kuongoza kwa maambukizi ya ukimwi bado ilionekana inafaa kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia. Safari yote ya Mbeya mwanahabari-makenika ameshindwa kuona mambo chanya kama utekelezaji wa vitendo wa sera ya kilimo kwanza, hakupishana na malori yanayokimbilia Dar es Salaam yakiwa yamesheni vyakula na matunda anuai. Hakushanga hali ya hewa safi tofauti na hali ya Dar es Salaam iliyojaa sumu. Hakuona milima na mabonde yanayohitaji wawekezaji wa aina-aina. Hakuona ukarimu wa watu, wenyeji na wageni. Hakufurahia maji yasiyokatika. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni.

Hitimisho.

Nina wasiwasi na ufahamu na uwezo wa kufikiri wa mwanahabari-makenika. Sidhani kuwa hajaenda shule kwani kusoma na kuelimika sio lazima vikatangamana. Nadhani ni wakati sote tuliolazimishwa kuisoma (ndio katutumia kwa lazima)ripoti hii tukaiangalia kwa jicho la pili. Hata majibu yangu haya pia yanahitaji upembuzi makini. Sio lazima yakawa ya kweli kwani nimeandika kwa kuzingatia maslahi ya kimkoa zaidi. Lakini nachelea mwanahabari alikuwa na nia ya kuupa mkoa wa taswira potofu zaidi ya ile iliyopo. Ni kweli mawazo yake ni baadhi ya changamoto sio tu katika Mbeya bali pia nchi nzima. Wapi hakuna mauzauza kama haya. Huko Dar es Salaam ambako mwanahabari- makenika anatoka/anaishi ndio usiseme!

Labels:

6 Comments:

At 10:08 AM, Blogger Fadhy Mtanga said...

Kaka John nakushukuru sana kwa haya uliyoyasema. Mimi ni mmoja ya watumiwa barua hiyo na huyo mwandishi-makenika ama fundi nini sijui. Mimi nimekuwa mkazi wa Mbeya tangu nasoma hadi katikati ya mwaka 2006 nilipokuja huku jiji kubwa kusaka mkate. Lakini nimejijengea utamaduni wa kurudi Mbeya kila baada ya miezi mitatu.
Kwa desturi yangu, nikiwa Mbeya hupenda kwenda viwanja tofauti vya starehe nikiwa na rafiki zangu ambao bado wamo humo.
Niliposoma barua ya mshikaji wetu nilijaribu kuvuta taswira. Lakini imegoma.
Ukweli utabaki kuwa ukweli. Ni kweli maambukizi yapo juu mkoani Mbeya. Lakini nimekerwa na tabia ya mwandishi-fundi huyu kwa kutia chumvi kiasi kikubwa. Kawadhalilisha sana dada zetu. Napenda kumfahamisha, Mbeya hakuna ukahaba wa aina anayoisimulia. Nasema kwa sababu nikiwa Mbeya nakata sana mitaa. Nakubali kuwa mji wowote lazima kuna biashara ya ngono, lakini mshikaji wetu amejipa umaarufu uchwara kwa kuwadhalilisha dada zetu! Kwanza ukiangalia kwa makini utagundua yeye ndiye aliyekuwa na uroho wa wanawake. Chungua vizuri simulizi yake.
Napenda jamii ijifunze kuepukana na aina hii ya uandishi.
Namkumbusha mwandishi-fundi huyu umuhimu wa kukifahamu kile akiandikacho. Asiandike tu ili nawe aonekane anajua kitu.

Kaka Mwaipopo, naomba kutoa hoja.

 
At 12:28 PM, Blogger Masangu Matondo Nzuzullima said...

Naona habari hii ilitumwa kwa wanablogu karibu wote. Huyu Mwanahabari ni nani? Na lengo hasa la makala haya lilikuwa ni nini?

Mtu yeyote anayajiamini na mwenye uhakika na anachokisema hataogopa kutumia jina lake kamili. Nilipoona tu jina la mwandishi, sikuipa uzito sana habari hii na kusema kweli sikumaliza hata kuisoma. Kuna maswali mengi ya kichambuzi yanayoweza kuzushwa hapa lakini inavyoonekana habari hii ni ya "kipiga stori" zaidi kuliko kichambuzi. Nadhani haisitahili hata kuchambuliwa!

 
At 2:31 AM, Blogger mike pima said...

Unajua kitu kimoja huwezi fahamu tabia mbaya za mke wako wala dada yako majirani ndo wanajua kwahio kama mtu akielezea ubaya fulani usiseme haupo chakufanya chunguza kuna baadhi ya mambo kazungumza sio siri yapo mbeya na sio mbeya tu miji mikubwa yate

 
At 12:09 AM, Blogger Yasinta Ngonyani said...

Ni swali nzuri sijui alitaka nini kujisifu au kudharau....

 
At 7:08 AM, Blogger yusuf said...

Huyu bwana nina wasiwasi na elimu yake! Sidhani kama anaweza kumconvice hata mtu ambaye hajawahi fika mbeya kwamba hayo ndiyo yanayojiri.Ni kweli makanisa ni mengi lakini si kiwango hicho mfano mdogo tu palepale stand kuu piga hatua kuelekea upande wowote kama kweli hatua 30 utakutana na kanisa? ukweli ni kwamba tanzania nzima kila ukienda mkoa wowote utakutana na malaya wewe unaenda kuchukua gesti uwanja wa fisi halafu unalalamika malaya wanakusumbua tafuta hoteli za maana kama wewe si muumini wa gono,Namba za simu uwape mwenyewe halafu unadai wanakufuata,kama si muumini wa hayo mambo unatoa namba za nini? Stori yako inanipa wasiwasi wa darasa lako huenda ndiyo uwezo wako wa kufikiri huo sababu hatuwezi jua umesoma kiasi gani ila wewe mwenyewe ndiyo unatuthibitishia kuwa unahitaji ukalie dawati.

 
At 9:45 AM, Blogger Chars said...

he's true,, na Navoijua Mbeya haya mambo yapo haina haja ya kuitetea..makanisa kila kona haina haja ya kupinga hili swala.. mnakera af wazinzii ad kinyaa haa!!!makanisa wao.. uchawi wao.. mahubiri kila mtaa wao.. kuchunana NGozo wao khaa!!

 

Post a Comment

<< Home